IGP Wambura afanya mabadiliko makamanda wa polisi

0
18

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura, amefanya mabadiliko madogo ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi baada ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan kuteua na kuwapandisha vyeo baadhi ya maafisa mwezi Julai mwaka huu.

Naibu Kamishna wa Polisi, Saleh Ambika amehamishwa kutoka Kitengo Maalumu cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai kwenda kuwa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuchukua nafasi ya Kamishna Faustine Shilogile aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo ambaye aliteuliwa na kupandishwa cheo kuwa Kamishna wa Kamisheni ya Polisi Jamii.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Philemon Makungu amehamishwa kutoka Mkuu wa Operesheni mkoa wa Kigoma kuwa kamanda wa polisi wa
mkoa huo kuchukua nafasi ya Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai ambaye alipandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Janeth Magomi amehamishwa kutoka kamanda wa polisi mkoa wa Songwe kwenda kuwa kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, kuchukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi George Kyando ambaye amehamishiwa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai, Makao Makuu ya Polisi Dodoma.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Alex Mukama ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Shinyanga amehamishwa kwenda kuwa kamanda wa polisi mkoa wa Songwe.