IMF yaionya Kenya kuhusu kupokea mkopo mpya kutoka UAE

0
32

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeonya kuhusu mpango wa Kenya kukopa mkopo wa dola za Marekani bilioni 1.5 [takriban TZS trilioni 4] kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), likionya kwamba mkopo huo unaweza kuiweka Kenya kwenye hatari ya matatizo ya kifedha kutokana na mabadiliko ya sarafu za kigeni.

Julie Kozack, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa IMF, ameshauri kwamba Kenya itumie mkopo huo kama sehemu ya mkakati mpana wa kifedha wa kupunguza utegemezi wa madeni na kukabiliana na changamoto za kifedha zinazojitokeza.

“Tunathamini kuwa Kenya ina hatari kubwa ya matatizo ya deni, hivyo mkopo mpya unapaswa kuzingatiwa katika muktadha wa mkakati wa kifedha wa kina wa kupunguza hatari za deni, huku pia ikishughulikia changamoto za kifedha zinazojitokeza,” ameeleza.

Kenya imekubaliana kupokea mkopo huo kutoka UAE kwa awamu, ambapo Waziri wa Fedha, John Mbadi, alifichua kuwa mazungumzo ya mkopo huo yanaendelea na ukopaji huo unategemewa kuwa na riba ya asilimia 8.25 na kwa muda wa miaka saba.

Hata hivyo, amesema kuwa mkopo huo ni rahisi zaidi ukilinganishwa na Eurobond walioukopa hapo awali wenye riba ya asilimia 10.7.

Katika jitihada za kuepuka kuvuka mipaka ya kukopa iliyowekwa na IMF, serikali ya Kenya inapanga kugawa mkopo huo kwa awamu, na awamu ya kwanza ya Ksh bilioni 90 [TZS trilioni 1.8] inatarajiwa kutolewa mwezi Januari, huku kiasi kilichosalia kikiwekwa kwenye akaunti za Kenya hapo baadaye.

Kenya na UAE zimekua na uhusiano mzuri wa kibiashara, ambapo Februari mwaka huu mataifa hayo mawili yalitia saini makubaliano ya kibiashara (CEPA), ambayo yatawezesha Kenya kuuza bidhaa zake katika soko la Asia na Mashariki ya Kati. Hii ni hatua muhimu katika kujenga uchumi wa Kenya, hasa katika sekta ya mafuta, ambapo Kenya ni miongoni mwa nchi za kwanza za Afrika kuanzisha mazungumzo ya kibiashara na UAE.

Hata hivyo, tangazo la mkopo huu limeathiri bei ya shilingi ya Kenya, ambayo ilishuka kidogo mwishoni mwa Oktoba, kabla ya kurejea kwenye kiwango cha 129 kwa dola moja, ambapo imebakia kwa zaidi ya miezi miwili.

Send this to a friend