Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeipongeza Tanzania kwa namna inavyosimamia sera zake za uchumi na fedha ikiwemo kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa IMF anayesimamia Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika, Willie Nakunyanda alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF na Benki ya Dunia, ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Makao Makuu ya Taasisi hiyo, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Kiongozi huyo amesema kuwa nchi nyingine za Afrika zinalo la kujifunza kuhusu usimamizi wa uchumi na sera za fedha kutoka Tanzania kutokana na umahiri wake katika eneo hilo ambapo nchi imekuwa imara kiuchumi licha ya misukosuko mingi ya kiuchumi na kijamii inayojitokeza duniani.