Instagram yafuta ujumbe wa Askofu Gwajima kuhusu uhusiano wa corona na 5G

0
42

Mtandao wa Instagram umeufuta ujumbe wa video uliowekwa na Askofu Josephat Gwajima unaoeleza kuwa janga la virusi vya corona lina uhusiano na juhudi za kusambaza teknolojia ya mawasiliano ya 5G.

Kampuni ya Facebook ambayo ndiyo inamiliki mtandao huo imesema kuwa umeufuta ujumbe huo kwa sababu unakiuka kanuni na masharti ya mtandaoni.

Katika ujumbe huo uliochapishwa mtandaoni mwezi Mei mwaka huu Askofu Gwajima alikuwa ameishauri Tanzania kutoikubali teknolojia hiyo ya 5G.

“Wote walioathirika vibaya wana teknolojia ya 5G, hapa [Tanzania] hatuna. Ushauri wangu ni kuwa Tanzania isianzishe mawasiliano ya 5G kwa sasa hivi,” alieleza Gwajima.

Facebook imesema imekuwa ikifuta jumbe mbalimbali ambazo zimekuwa zikipotosha jamii kuhusi masuala mbalimbali ikiwamo janga la virusi vya corona.

Shirika la Afya Duniani (WHO) pia limewahi kukanusha uvumi kuwa virusi vya corona vinaweza kusambaa kupitia mawimbi ya redio au mitandao ya simu.

Send this to a friend