Intaneti kwa njia ya simu inavyochagiza ukuaji wa uchumi jumuishi
Kisaka Msuya, UDBS
Hivi karibuni Benki ya Dunia imetangaza kuwa Tanzania imeingia rasmi kwenye uchumi wa kati ikiwa ni miaka mitano kabla ya kufikia ukomo wa muda uliokuwa umewekwa na serikali yaani 2025.
Tanzania imefanikiwa kufikia hatua hii kutokana na ukuaji imara wa uchumi. Kwa mfano, mwaka uliopita Tanzania ilirekodi ukuaji wa uchumi kwa asilimia 7, hivyo kusaidia kuendelea kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.
Mafanikio ya nchi kufikia uchumi wa kati ni kitu cha kujivunia sana. Lakini ni muhimu kuhakikisha kuwa jitihada zaidi zinafanyika ili kuhakikisha kuwa faida ya mafanikio ya nchi yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.
Uchunguzi wa hivi karibu wa wanazuoni kutoka Marekani umeonesha kuwa teknolojia ya kidigitali imekuwa nyenzo muhimu sana ya kuzisaidia nchi za Afrika kufikia ukuaji wa uchumi jumuishi. Utafiti wao umedadavua kuwa upatikanaji wa huduma ya intaneti kwenye simu hukuza upatikanaji wa taarifa za fursa mbalimbali kujikwamua kiuchumi, mtandao wa ajira, fursa za kazi na kipato jumuishi.
Kwa miaka ya hivi karibuni usambaaji wa huduma ya intaneti nchini umekua sana na kufikia asilimia 46. Ukuaji huo umechangiwa pia kwa kiasi kikubwa na kampuni za watoa huduma za mawasiliano ya simu nchini.
Watoa huduma hawa wamefanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa wanaziba ombwe la upatikanaji wa mtandao wa intaneti kati ya maeneo ya mjini na vijijini. Sasa ni wazi kuwa kusaidia jamii za vijijini kupata huduma ya intaneti ya uhakika ni jambo muhimu sana katika kupunguza utofauti kati ya jamii hizo mbili.
Mbali na hilo, kuwa na huduma ya intaneti ya uhakika ni njia muhimu ya kusaidia kufanikisha uwepo wa fursa za kiuchumi kwa ambao walikuwa wameachwa nyuma. Kwa mfano, huduma ya fedha ya Kampuni ya Tigo (Tigo Pesa) inawasaidia wale wote ambao hawakuwa na uwezo wa kupata huduma za benki kama kupata mikopo na kuweka akiba, ambayo mwisho wake inasaidia kukuza huduma ya fedha jumuishi.
Tigo inaendelea kufanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa inaziba utofauti wa kidijitali uliopo sasa. Simu yao mpya ya gharama nafuu ya Kitochi 4G inamuwezesha mtumiaji kukamilisha mawasiliano pamoja na kuperuzi mitandao ya kijamii kama vile Facebook na WhatsApp.
Wakati nchi ikiwa imefungua ukurasa mpya kuelekea ukuaji mkubwa wa uchumi na maendeleo, tuangazie kwa mapana namna ambazo kampuni za simu zinaweza kuendelea kuwa na mchango mkubwa katika kufikia mafanikio.
Kwa kuwekeza katika miundombinu ya kizazi kijacho, kampuni za mawasiliano ya simu zinaweza kuendelea kuboresha usambazwaji wa huduma ya intaneti na kuhakikisha Watazania wengi zaidi wananufaika na huduma za simu. Tuendelee kuwa na matumaini kuwa sekta hii itapata msaada inaohitaji kupitia sheria na kanuni rafiki na vichocheo vya uwekezaji kwani kwa kufanya hayo, tutaweza kukahakikisha kuwa mafanikio yanawagusa Watanzania wote.