Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia mtoto mwenye umri wa miaka 14 (Jina limehifadhiwa) Mkazi wa Kihesa Kilolo B kwa tuhuma za kuwalawiti watoto wenzake 19.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, amesema mtoto huyo amekamatwa baada ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Kihesa Kilolo B, Elizabeth Lugenge kutoa taarifa ya kuwepo kwa watoto watatu wanaosoma katika shule ya Msingi Igeleke kulawitiwa.
“Baada ya mahojiano, watoto hao walikubali na kuwataja wenzao watano. Na hao watano walipohojiwa wakawataja wengine watano hivyo kufanya idadi ya watoto 13. Mtuhumiwa alipohojiwa alikubali na akawataja watoto wengine sita, wakawa 19,” amesema Bukumbi.
Aidha, Kamanda Bukumbi ameeleza kuwa mtuhumiwa alisema kuwa ameanza kufanya matukio ya ulawiti mwaka 2019, eneo alilokuwa anatumia kulawiti wenzake ni eneo la Pagani ambalo liko karibu na nyumbani kwao.
Kamanda Bukumbi ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akichukuwa fedha kwa bibi yake Sauda Muhammad (57) ananunua pipi kama mbinu ya kuwapata wenzake ili awafanyie kitendo hicho wakati walipokuwa wakienda nyumbani kwao kuangalia TV.
Hata hivyo imeelezwa kuwa watoto wote waliotajwa walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa na walipofanyiwa uchunguzi ukabaini kuwa wamelawitiwa. Kesi nane tayari zimefunguliwa na upelelezi umeshakamilika hivyo mtuhumiwa anatarajia kufikishwa mahakamani.