Ishara 10 kubaini mtu anakudanganya wakati wa mazungumzo

0
20

Mara ngapi umewahi kushangaa au kujiuliza kwanini mtu anakudanganya? Watu hudanganya kwa sababu tofauti, inaweza kuwa kuficha vitu vibaya walivyofanya au hutumia uongo  kumshawishi mtu mwingine.

Zifuatazo ni dalili za kutambua mtu anakudanganya wakati wa mazungumzo;

1. Mwenendo wa kichwa chake

Mtu anaezungumza uongo akiulizwa swali mara nyingi hujibu kwa kutikisa kichwa chake nyuma, pembeni, na muda mwingine huinamisha kichwa chini kama ishara ya kujisikia vibaya kwa kitu anachofanya.

2. Kuhema

Dalili hii si rahisi sana kuitambua ila unaweza kugundua kwa kutazama mtu anavyopandisha mabega yake na kupumua kwa nguvu na hata sauti yake hubadilika na kuwa kama haitoki vizuri, mabadiliko hayo kwenye kuhema husababishwa na hofu.

3. Utulivu

Mara nyingi tunapokuwa tunazungumza mwili huwa na mwenendo tofauti tofauti, lakini si rahisi kwa mtu anapozungumza uongo. Mara nyingi mtu anapozungumza uongo hutulia kama ishara ya kuwa yuko tayari kwa ajili ya mapambano au kukimbia.

4. Kurudia rudia vitu

Hii ni ishara kwamba hana uhakika na anachokizungumza na anatumia kama sehemu ya kushawishi akili yake kuwa yuko sahihi kwenye kitu anachokizungumza pia hutumia kama mbinu ya kukusanya mawazo ndani ya kichwa chake.

5. Kutoa taarifa nyingi

Sio rahisi kwa mtu anapozungumza uongo kutoa majibu ya moja kwa moja anapoulizwa swali, mara nyingi majibu atakayotoa yatakuwa na taarifa nyingi zaidi ya kile alichoulizwa ili kumuaminisha anayemuuliza kuwa yeye ni muwazi na hana kitu cha kuficha.

6. Kujishika shika na kujificha

Mikono hutumika kushika vitu vinavyomzunguka na kujiziba sehemu za midomo, hii ni ishara ya kwamba analazimishwa kujihusisha au kuongelea kitu ambacho hana utayari nacho.

7. Kujificha zaidi

Binadamu anapokuwa anajihusisha na vitu hatari mara nyingi hujifunika au kuficha maeneo kama kichwa, kifua na koo. Hivyo hivyo kwa mtu anapokuwa anazungumza uongo hufunika na kuficha zaidi maeneo hayo ishara ya kuwa anajihusisha na mambo magumu.

8.  Kutikisa miguu

Mtu anapozungumza uongo hutikisa au kutingisha miguu yake kuonesha hisia zake kuwa hayuko sawa na mazingira aliyopo na anatamani kuondoka.

9. Kukosa maneno

Hisia ambazo mtu anapata anapozungumza uongo hupelekea kukosa maneno ya kuongea  na kufanya mazunguzo kuwa magumu na muda mwingine huanza kung’ata midomo yake.

10. Kupepesa macho

Kupepesa macho ni kawaida kwa mwanadamu, binadamu wote hupepesa macho bila kufikiria kwanini anapepesa macho. Hii ni tofauti kwa mtu anapozungumza uongo kwani yeye hupepesa macho zaidi kama ishara ya kujishtukia na kutotaka kukutana macho kwa macho na mtu anayezungumza nae.