
Kila binadamu anahitaji kufanya kazi ili kuendesha maisha yake na maisha ya watu wanaomtegemea. Ikiwa kazi unayoifanya inakwenda kinyume na wewe, pengine ni wakati sahihi wa kuachana na kazi hiyo.
Hizi ni ishara zinazoonesha kuwa ni muda wa kuachana na kazi unayoifanya;
1. Huna tena furaha kazini
Unapojikuta unaamka asubuhi ukiwa na huzuni au hofu ya kwenda kazini mara kwa mara, hiyo ni dalili kuwa umechoka au kazi hiyo haikufai tena kiakili wala kihisia.
Ukosefu wa furaha kazini huathiri afya ya akili, ufanisi na hata maisha binafsi.
2. Hakuna ukuaji wa kitaaluma
Ukigundua kuwa huna nafasi ya kupanda cheo, kujifunza kitu kipya, au kukua katika taaluma yako, basi kazi hiyo inaweza kuwa kikwazo kwa maendeleo yako.
3. Mazingira ya kazi ni mabaya
Unapojikuta unazungukwa na majungu, kutothaminiwa, au kukumbana na ubaguzi wa wazi au wa kificho, unakuwa kwenye mazingira yasiyo salama kisaikolojia.
4. Kazi hailingani na maadili yako
Kama kazi inahusisha vitendo ambavyo vinapingana na misingi yako ya kiimani, utu au heshima, hiyo ni ishara ya kutafuta mwelekeo mwingine. Mfano: Kampuni inahusishwa na ufisadi, unalazimishwa kusema uongo kwa wateja, au kutoa huduma za kibaguzi.
5. Unafanya zaidi ya majukumu yako bila kutambuliwa
Ukibeba majukumu ya watu wengine au kufanya kazi kubwa isiyoambatana na malipo au kutambuliwa, na hali hiyo imekuwa ya kudumu, hiyo ni dalili ya kukosa kuthaminiwa.
6. Afya yako inazorota kwa sababu ya kazi
Kama kazi imekuwa chanzo cha uchovu mkubwa, presha, au hata maradhi kwa mfano usingizi haukutoshi, kula kwa shida, au huna muda wa familia hupaswi kuendelea na kazi hiyo.
7. Unalipwa chini sana kuliko kiwango cha soko
Kama mshahara wako ni mdogo ukilinganisha na wengine wa nafasi yako, na huna matumaini ya nyongeza, unaweza kuangalia kazi nyingine yenye thamani zaidi.
8. Kazi inakunyima muda wa maisha binafsi
Kama kazi inachukua muda mwingi mno hadi unakosa muda wa familia, marafiki, mapumziko, au mambo unayoyapenda, hiyo si kazi yenye afya kwa maisha ya muda mrefu.
9. Kazi haina maana tena kwako
Unapojikuta huelewi kwa nini unafanya kazi hiyo, huoni mchango wowote, au unakosa msukumo wa ndani kabisa, ni wakati wa kutafakari upya.
10. Umeanza kupata fursa nzuri zaidi mahali pengine
Kama umeanza kupata maombi ya kazi nyingine bora, au una ndoto imekuja (mfano kuanzisha biashara, au kurudi shule), huo unaweza kuwa wakati wa kuondoka kwa heshima.








