Israel imeahidi kuongeza jitihada kuwapata Watanzania wawili waliotoweka tangu kuanza kwa mapigano kati ya Hamas na Israel, ambao ni sehemu ya kundi la vijana waliokwenda nchini humo kwa ajili ya mafunzo ya kilimo cha kisasa.
Ahadi hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Eli Cohen katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, January Makamba ambaye pia alitumia wasaa huo kueleza msimamo wa Tanzania juu ya mapigano hayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Watanzania wawili, Joshua Loitu Mollel and Clemence Felix Mtenga, ambao walikuwa nchini humo kwa mafunzo ya kilimo, wametekwa na kundi la Hamas na wanashikiliwa katika eneo la Gaza.
Kuhusu mapigano hayo, Tanzania imehimiza kutumika njia ya mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yenye lengo la kufanikisha uwepo wa mataifa mawili, kama suluhisho la kudumu la mgogoro wa zaidi ya miongo nane kati ya pande hizo mbili.
Rwanda yaondoa sharti la visa kwa Waafrika wote
Mbali na kuhimiza mazungumzo ya amani, Tanzania imesisitiza kuzingatiwa kwa sheria za kibinadamu za kimataifa, hasa katika kuwalinda raia katika mapigano hayo pamoja na kusitisha mapigano ya kijeshi ili kuruhusu kufikishwa kwa misaada ya kibinadamu.
Mapigano kati ya Hamas na Israel yalichukua sura mpya Oktoba 7 mwaka huu baada ya kundi hilo kufanya kuishambulia Israel, hatua iliyopelekea Israel kujibu mashambulizi na kuzalisha mapigano ambayo yamedumu kwa mwezi mmoja sasa yaliyopelekea vifo vya maelfu ya raia na kuharibiwa kwa makazi.