
Zaidi ya Wapalestina 400, wameuawa katika mashambulizi mapya ya Israel ambayo yameonekana kuvunja makubaliano ya usitishwaji wa mapigano Gaza.
Hamas imeishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano ya usitishwaji wa mapigano yaliyowekwa mwezi Januari, huku Israel ikiilaumu Hamas kwa kukataa mara kwa mara kuwaachia mateka na kukataa juhudi za upatanishi.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu imetoa taarifa na kutangaza kuanzishwa tena kwa vita vya Israel dhidi ya Gaza.
Jeshi la Israel limeelezea mashambulizi hayo kama shambulio la kujihami kabla ya hatari, lililolenga kuzuia Hamas kujiimarisha upya na kushambulia Israel. Aidha limesema mashambulizi hayo yaliwalenga maafisa wa ngazi za kati wa kijeshi, viongozi wa Hamas, na miundombinu ya kigaidi ya kundi hilo.
Mashuhuda wamesema mashambulizi ya anga pia yalilenga nyumba na kambi za zinazowahifadhi raia kutoka kaskazini hadi kusini mwa Ukanda wa Gaza, huku vifaru vya Israel vikishambulia kwa mizinga katika maeneo ya mpakani.