Jafo: Zuio la matumizi ya mkaa na kuni haliwahusu wananchi

0
63

Serikali imetangaza kwamba katazo la matumizi ya kuni na mkaa litazihusu taasisi za umma na za binafsi pekee, na halitawahusu wananchi binafsi kama ambavyo imekuwa ikitafsiriwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema kuanzia Januari 31, 2024, taasisi zote za umma na za binafsi zinazotoa chakula na kuwalisha watu zaidi ya 100 kwa siku zinapaswa kusitisha matumizi ya kuni na mkaa, na taasisi zinazotoa chakula kwa watu zaidi ya 300 kwa siku zinapaswa kufanya hivyo ifikapo Januari 31, 2025.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kudhibiti uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti kwa kiwango kikubwa na pia kulinda afya za wananchi.

“Bahati mbaya sana baadhi ya watu walitafsiri lile tangazo tulilotoa mwezi wa nne wakawa na wasiwasi kuwa sasa itakuwaje hata mama n’tilie au majumbani watashindwa kupika, hapana si hivyo lengo letu ni kuanza kwa taasisi zenye watu wengi.

Sababu za Tanzania kuilipa kampuni ya Canada fidia ya bilionea 76

Ni kweli shule zetu ni watumiaji wakubwa wa kuni, nenda katika taasisi zetu nyingine utaona namna gani kuni zinatumika ndio maana tukatoa maagizo haya kwetu sisi wenyewe (taasisi za Serikali na taasisi binafsi) kwanza tuanze kujipanga katika hili na tutasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira,“ amesisitiza Dkt. Jafo.

Aidha, ameeleza kwamba matumizi ya kuni na mkaa yanaweza kuathiri afya ya watumiaji kwa kusababisha magonjwa yanayotokana na kuvuta hewa chafu, ambayo inaweza kuathiri mapafu na moyo na pia matumizi ya muda mrefu ya nishati hii pia yanaweza kusababisha magonjwa ya macho.

Send this to a friend