Jaji Mkuu ataja vigezo alivyotumia Rais Samia kumteua Jaji Siyani

0
22

Leo Rais Samia Suluhu Hassan amemwapisha Jaji Mustapha Siyani, kuwa Jaji kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, akiwa ni mmoja wa viongozi watatu walioapishwa, wengine wakiwa ni Sofia Mjema, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jaji Omar Makungu, kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Awali akizungumza baada ya uapisho huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma amesema kulikuwa na majaji 85 wenye uwezo wa kuteuliwa kushika wadhifa huo, lakini vigezo mbalimbali vimezingatiwa kumpata Jaji Siyani.

Amesema kigezo cha kwanza cha uteuzi ni ufahamu wa mahakama kiundani pamoja na miiko (traditions) yake. “Ukifahamu undani wa mahakama, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya maboresho.”

Amesema kuwa kigezo kingine ni mtu anayefahamu kuwa mahakama sio kisiwa, na kwamba inaingiliana na mihimili mingine, lakini aelewa mipaka ya mahakama na changamoto za mihimili mingine.

Prof. Juma amesema pia nafasi hiyo inahitaji mtu mwenye busara kwani ataongoza watu wakubwa na wadogo kuliko yeye.

“Busara, hekima, utu, ubinadamu ni jambo ambalo kiongozi yeyote katika nafasi yako anatakiwa kuwa nayo,” amesisitiza Prof. Juma.

Jaji Mkuu ametanabaisha kwamba nafasi hiyo pia inahitaji mtu anayejua mahakama inakwenda wapi, kwani majaji na mahakimu wanaweza wakapotelea kwenye kuandika hukumu lakini dunia inakwenda, hivyo lazima mtu aweze kuipeleka mahakama kuendana na wakati.

“Vile vile uelewe safari ya kwendea mahakama mtandao. Tumefanya uwekezaji mkubwa katika mahakama katika TEHAMA, sasa ni wakati wa kufanya uwekezaji ule uzae matunda,” ameeleza.

Aidha, amesema Jaji Kiongozi lazima aweze kujenga umoja kati ya watu kwenye nyanja mbalimbali kwani bila hilo mahakama haiwezi kusonga mbele, huku akimtaka kuwa na desturi ya kujifunza zaidi na kupokea ushauri kutoka kwa watu wengine.

Amesema anaamini Jaji Siyani akisimamia nguzo tatu za mahamakama ambazo ni utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, pili, upatikanaji na utoaji wa haki kwa wakati na tatu, kuimarisha imani ya wananchi, anaamini mhimili wa mahakama utasonga mbele