Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga ameshauri Rais Uhuru Kenyatta avunje bunge la nchi hiyo kutokana na kutokuwa na wabunge wanawake wakutosha.
Katika barua yake kwa Kenyatta, Maraga amesema kutokuwepo kwa wabunge wanawake wa kutosha ni ukiukwaji wa katiba na ubaguzi dhidi ya wanawake.
Katiba ya Kenya inaeleza kuwa jinsia moja haiwezi kuchukua zaidi ya mbili ya tatu ya viti vya ubunge. Hata hivyo, idadi ya wabunge wanawake ni chini ya 116, ikiwa ndio idadi ya chini zaidi ya wanaotakiwa kuwepo kati ya wabunge wote 350.
Jaji huyo amesema kuwa bunge limeshindwa au limepuuza kuweka sheria yakutekeleza takwa hilo la kikatiba, licha ya mahakama kutoa amri mara nne, na kutokana na hilo amemshauri Rais kulivunja bunge.
Kenya ilianza kutumia katiba mpya mwaka 2010 na sheria hiyo ya mbili ya tatu ya wabunge ilitakiwa kuanza kutimika miaka mitano iliyopita.
Kwa upande wake Spika wa Bunge, Justin Muturi amesema kuvunja bunge ni suluhisho lisilo na tija.
Baadhi ya wabunge nchini humo wamesema hakuna haja ya kuwekwa mkakati wa kuwawezesha wabunge wanawake kuongezeka bungeni, badala yake wagombee kwenye majimbo kama wafanyavyo wanaume.