
Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Milwaukee, nchini Marekani, Hannah Dugan, amekamatwa na maafisa wa FBI na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusaidia mhamiaji asiye na vibali kuepuka kukamatwa akimtorosha kupitia mlango wa siri.
Kulingana na nyaraka za mashtaka, maafisa waliovaa kiraia waliingia kwenye mahakama ya Dugan Aprili 18, 2025 kwa lengo la kumkamata Flores-Ruiz, raia wa Mexico, ambaye aliwahi kuondolewa Marekani mwaka 2013, lakini maafisa wa uhamiaji waligundua amerudi kinyume cha sheria baada ya kukamatwa kwa kesi ya unyanyasaji wa majumbani.
Baada ya kupewa taarifa na msaidizi wake kuwa maafisa wa serikali wapo, Jaji Dugan alichukizwa, akisema kuwa tukio hilo ni la ajabu, kisha aliwakabili maafisa hao na kuwataka waondoke.
Hata hivyo, mtuhumiwa Flores-Ruiz alikamatwa muda mfupi baadaye nje ya jengo la mahakama baada ya kukimbizwa kwa miguu na maafisa wawili waliokuwa karibu na chumba cha mahakama.
Jaji Dugan anakabiliwa na mashtaka mawili: kuzuia haki na kumficha mtu anayesakwa. Katika kesi yake, wakili wake amesema Jaji Dugan anasikitishwa sana na kukamatwa kwake na anapinga vikali, akisisitiza kuwa kukamatwa kwake hakukuwa kwa ajili ya usalama wa umma.