Jaji Warioba ashauri kura ya maoni ya katiba mpya kufanyika mwaka 2024

0
82

Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba ameishauri serikali kufanya kura ya maoni kuhusu uhitaji wa katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Jaji Warioba ametoa pendekezo hilo na kushauri kwamba kura hiyo ifanyike wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024, huku akisisitiza kwamba mchakato wa katiba hauzuii shughuli nyingine kuendelea kufanyika.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume iliyoandaa rasimu ya katiba kuanzia mwaka 2012 akizungumza na na gazeti la Mwananchi amesema kuwa mchakato wa katiba hiyo ulikaribia kwisha kwani tayari rasimu ilikuwa imepitishwa na Bunge la Katiba.

Ameongeza kwamba baada ya hapo hatua iliyokuwa inafuata ilikuwa ni kura ya maoni, lakini aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mwaka 2015, Jaji Damian Lubuva alisema walikuwa wakijiandaa na uchaguzi mkuu hivyo isingewezekana kufanyika kwa kura ya maoni na uchaguzi wakati mmoja. Aliomba zoezi hilo lisogezwe mbele, na hivyo walitarajia baada ya uchaguzi lingefanyika, lakini halikuwahi kufanyika tena.

Hata hivyo amesema kutokana na changamoto za UVIKO19 na hali ya uchumi, ni vigumu kukamilishwa kwa mchakato huo kwa sasa, hivyo amewashauri viongozi wa vyama vya siasa kukutana kuona namna ya kuendelea nao.

“Binafsi nadhani kura ya maoni inaweza kufanyika mwaka 2024 kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa. Kupunguza gharama tunaweza kuchanganya uchaguzii huo na kura ya maoni,” amesema Warioba.

Amesema hakuna haja ya kuanza upya mchakato huo kwani taarifa zote muhimu zilikusanywa.

Akizungumzia uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amesema kwamba hakuna haja ya kusubiri katiba mpya kwa sababu kinachohitajika kufanyika ni mabadiliko ya sheria tu, ambayo hayahitaji uwe na katiba mpya ndio upitishe.