
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeahirisha kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu hadi Agosti 18, 2025, itakapotoa amri kuhusu ombi na pingamizi la kurusha mubashara ushahidi katika kesi hiyo.
Upande wa Jamhuri umeiomba mahakama kutorusha mubashara mwenendo wa wakati mashahidi wakiwasilisha ushahidi wao mubashara ili kuepusha mashahidi kujulikana, ombi ambalo limepingwa na upande wa utetezi.
Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga amesema kuwa mashahidi wanaohusiana na kesi hiyo watakuwepo mahakamani, lakini taarifa zao hazitarushwa hewani kutokana na amri ya mahakama.
“Hao watu anaotaka wawepo hapa mahakamani watakuwepo, ila amri ya mahakama imezuia uchapishaji wa taarifa zao,” ameeleza.
Ameongeza kuwa “Ombi letu, pamoja na nia njema ya mahakama kuonesha mwenendo wa shauri kwenye vyombo vya habari, ni kwamba yafuatwe maagizo ya Mahakama Kuu. Ikiwa mshtakiwa atasomewa mashtaka, basi iwe kwenye mahakama ya wazi lakini bila matangazo ya moja kwa moja.”
Kwa upande wa Lissu amesema marejeo aliyotumia wakili wa serikali yanataka upande wa mashitaka uondoe vielelezo vitakavyopelekea mashahidi kutambuliwa, na siyo kuzuia kesi kurushwa mubashara.







