January Makamba atoa neno la mwisho baada ya kung'olewa uwaziri

0
23

Mbunge wa Bumbuli, January Makamba ametoa kile alichokiita neno lake la mwisho katika hatua nzima ya yeye kutenguliwa uwaziri, ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake kwa viongozi wa juu kwa namna walivyoonesha imani kwake na kumsimamia kipindi chote alichoongoza wizara.

Makamba ambaye amejizolea umaarufu kufuatia namna alivyosimamia usitishwa wa matumizi ya vibebeo (mifuko) ya plastiki, uteuzi wake kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ulitenguliwa jana.

Kufuatia utenguzi huo Rais alimteua George Simbachawene kushika nafasi hiyo. Kupitia ukurasa wake wa Twitter Makamba aliandika kuwa ameyapokea kwa moyo mweupe mabadiliko hayo, na kuwa angeongea siku za mbeleni.

Baada ya viongozi wateule kuapishwa leo, Makamba amewashukuru Rais, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu kwa usimamizi wao kwa muda wa takribani miaka minne aliyoongoza Wizara ya Muungano na Mazingira.

Neno la Mwisho kwenye hili: Namshukuru Rais kwa kuniamini, Makamu wa Rais kwa kunielekeza, Waziri Mkuu kwa kunisimamia, na Team (timu) ya Ofisi ya Makamu wa Rais (VPO), Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mawaziri wote kwa ushirikiano. Nampongeza Hussein Bashe na George Simbachawene kwa kuaminiwa. Nawatakia heri na kuwaahidi ushirikiano wangu wa dhati.

Maneno hayo yamekuja saa chache baada ya Rais kuelezwa kuwa hakufurahishwa na mwenendo wa wizara hiyo ambapo alitaja mambo yaliyomfanya asifurahie kuwa ni kucheleweshwa kwa vibali kwa wakwekezaji, kuwepo miradi hewa, kutoonekana kwa matokeo ya fedha zinazoelekezwa kwenye mazingira, na kucheleshwa kwa katazo la mifuko ya plastiki.

Nakumbuka suala la mifuko ya plastiki limechukua muda mrefu, karibu miaka minne, nimetia saini halikutekelezwa, Makamu wa Rais akazungumza weee halikutekelezwa, Waziri Mkuu akazungumza Bungeni halikutekelezwa, mpaka mwishoni mwishoni hapa nilipotoa amri ya lazima ndipo likaanza kutekelezwa, sasa usiende kufanya hivyo wewe (Mhe. Simbachawene).

Ras amemtaka Simbachawene kuhakikisha fedha nyingi zinazoelekezwa katika masuala ya mazingira zinaleta matokeo ya kuboresha mazingira, vibali vya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) haviwi kikwazo cha uwekezaji na kutekeleza maagizo yanayotolewa na Serikali kwa wakati.

Send this to a friend