Je, kuna uwezekano wa binadamu kuishi mwezini?

0
23

Kuna juhudi za kisayansi na kiufundi zinaendelea kuchunguza uwezekano wa binadamu kuishi mwezini siku zijazo. Shirika la Anga za Juu la Marekani (NASA) na shirika nyingine za anga za juu zimefanya misafara kadhaa kwenda mwezini tangu miaka ya 1960, na hivi karibuni NASA, wakishirikiana na SpaceX, wanatarajia kuwashusha wanaanga mnamo mwaka 2024.

Afisa wa NASA, Howard Hu, ambaye anaongoza mpango wa vyombo vya anga vya juu vya Orion kwa shirika hilo, anasema wanadamu wanaweza kukaa kwenye mwezi, lakini pia makazi yanahitajika ili kusaidia misheni za kisayansi zinazofanyika.

Mazungumzo mbalimbali ya kujenga vituo vya kuishi mwezini yamekuwa yakiendelea. Hii inaweza kuhusisha kutumia malighafi zinazopatikana kwenye mwezi kwa ujenzi au kutuma vifaa kutoka duniani. Watafiti wanasema vituo hivyo vitasaidia kufanya utafiti wa kina pamoja na kutuma wanadamu kwa muda mrefu zaidi.

Baadhi ya mijadala inasema, ikiwa tunaweza kutumia rasilimali za mwezini kama vile maji na oksijeni iliyoko kwenye miamba ya mwezi, pengine kuna uwezekano wa kuweza kuishi mwezini.

Nchi 10 za Afrika zenye intaneti yenye kasi zaidi

Mbali na hayo, kuishi mwezini kumetajwa kuwa na changamoto za kiafya na za usalama, kama vile athari za muda mrefu za mionzi ya cosmic, hii inawapa nafasi watafiti kutafuta ufumbuzi zaidi.

Shirika la Habari la BBC limetaarifu kwamba baadhi ya watu tayari wamenunua maeneo mwezini wakiamini kwamba katika miaka 50 au 100 ijayo, makao ya binadamu yanaweza kuanzishwa huko na hivyo kutoa urahisi kwa familia zao kupata maeneo, jambo ambalo limezua majadiliano ikiwa ni sahihi kufanya hivyo au la.

The Lunar Registry ni kikundi cha kimataifa cha wanasheria ambacho kinafanyakazi ya kutafuta makazi, kufanya utafiti, na kubinafsisha maeneo kwenye mwezi kwa gharama kubwa ambapo wengi wameeleza kuwa kitendo cha kununua eneo mwezini ni upotezaji wa pesa.

Swali ni: Je, ikiwa umepata nafasi ya kununua eneo mwezini, utafanya hivyo?