Je! Ni wakati sasa CAF ifute ushindi wa goli la ugenini?

0
14

Baada ya Klabu ya Yanga kuukosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kigezo cha ushindi wa goli la ugenini aliopata USM Alger kwenye dimba la Benjamin Mkapa, licha ya kugaragazwa kwenye ardhi ya kwao nchini Algeria, baadhi ya wadau wa michezo wamelalamikia utaratibu huo wakidai uondolewe kwani umepitwa na wakati.

USM Alger ilifanikiwa kushinda magoli 2-1 dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Yanga ikifanikiwa kushinda goli 1-0 dhidi ya USM Alger ugenini, hivyo kanuni za CAF zikaitambua USM Alger kama bingwa kwa kigezo cha kuwa na magoli mengi (2) ya ugenini huku Yanga ikiwa na goli moja.

Akizungumza na Swahili Times Mchambuzi Jemedary Said amesema goli la ugenini ni kanuni ambayo imekuwa ikitumika karibu kila mwaka, hivyo Watanzania wanapaswa kutokuweka hisia zao kwa timu na kujielekeza zaidi kwenye sababu za kwanini timu ilikubali kufungwa magoli mengi nyumbani.

“Mpira wa Afrika kupata bao ugenini sio mchezo, kwa sababu kuna vitu vingi mno nje ya kiwanja na ndani ya kiwanja ambavyo vinajaribu kumvuruga mgeni, ni vingi mno. Kwahiyo haikuwa kwa bahati mbaya kwamba timu inayopata goli la ugenini katika mazingira ya sare ihesabike mara mbili, na hii haikuwa kwetu tu,” amesema.

Karia: Mimi sio mwanachama wa Simba

Kwa upande wake mchambuzi Geoffrey Lea (Jeff Lea) amesema Watanzania wanapaswa kukubali kuwa USM Alger ilikuwa bora kuliko Yanga, na kwamba kama sheria ya goli la ugenini ingeondolewa, huenda kusingekuwa na mabadiliko yoyote kwenye matokeo mara baada ya timu hizo kwenda hatua ya matuta.

“Kama Yanga wangeshinda mechi yao hapa au wangetoka sare, leo huu mjadala usingekuwepo kabisa, kwahiyo tusiingie katika mjadala wa kutaka kubadilisha sheria ‘ku-hide incompetence’ [kuficha udhaifu. Ukipoteza mechi ya kwanza kabisa mpongeze aliyeshinda, usiweke visingizio,”  ameeleza Jeff Lea.

Naye Mchambuzi Shafii Dauda amesema kanuni hiyo ya CAF imepitwa na wakati na haoni mantiki ya uwepo wake kutokana na mabadiliko mengi yanayofanyika katika tasnia ya mpira.

“Kwa muda mrefu nimekuwa pia nikizungumzia kuhusu kutokubali goli la ugenini. UEFA walipobadili na kuifuta, mimi nilifurahi kwa kweli, kwahiyo nikawa nategemea na CAF wangeweza kufuata nyayo hizo hizo za UEFA waweze kuliondoa, kwa hiyo mimi sioni mantiki ya hilo goli la ugenini,” amesema Dauda.

Akihitimisha mchambuzi George Ambangile amesema Afrika inapaswa kubadili vitu kutokana na mazingira yalivyo, hivyo haoni shida yoyote kwa goli hilo kubaki au kuondoka.

Send this to a friend