Jela miaka 30 kwa kuoana dada na kaka ili wakuze ukoo

0
26

Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imewahukumu ndugu wawili Mussa Shija, (33) kwenda jela miaka 20, na Hollo Shija (35) kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kuishi pamoja kama mke na mume.

Hukumu hiyo imetolewa August 14 mwaka huu na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Enos Misana baada ndugu hao wawili ambao wote ni wakulima na wakazi wa Kijiji Cha Mandang’ombe Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kupatikana na hatia.

Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mashitaka ya Taifa wilaya ya Maswa, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Vedastus Wajanga ameeleza kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo tarehe na miezi tofauti kati mwaka 2018 hadi Julai 31, 2024 katika kijiji cha Mandang’ombe wilayani humo.

Mwendesha Mashitaka huyo aliielezea mahakama kuwa washtakiwa ni ndugu wa damu kwa maana ya kaka na dada na katika mahusiano yao walikuwa wakiishi kama mke na mme na wamebahatika kupata mtoto mmoja mwaka 2022 ambae jina lake limeifadhiwa.

Washtakiwa waliomba mahakama iwapunguzie adhabu kwani ni wakosaji wa mara ya kwanza na wanafamilia inawategemea na kwamba kitendo walichokifanya wao hawakujua kuwa ni kosa kwani waliambiwa na babu yao mzaa baba kuwa ili wadumishe mila za ukoo wake wanatakiwa wao waoane.