Jenerali Tchiani aapishwa kuwa Rais wa Mpito wa Niger

0
5

Kiongozi wa Jeshi la Niger, Jenerali Abdourahamane Tchiani ameapishwa kuwa Rais wa Mpito wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano

Uamuzi huo umevunja juhudi za Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ambazo zilihimiza kurejeshwa haraka kwa utawala wa kidemokrasia baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Mahamane Roufai, Katibu Mkuu wa Serikali ya Niger, kipindi cha mpito kilianza rasmi siku ya Jumatano na kitakamilika mwaka 2030, ambapo Tchiani atakuwa ameongoza Niger kwa karibu miaka saba.

“Kipindi cha mpito kimewekwa kuwa miezi sitini kuanzia siku ya kutangazwa kwake. Hata hivyo, muda huu unaweza kubadilika kulingana na hali ya usalama wa nchi, mageuzi, na ratiba ya Jumuiya ya Nchi za Sahel,” amesema Roufai.

Jenerali Tchiani ameongoza nchi hiyo tangu 2023, baada ya kumuondoa madarakani Rais mteule wa Niger, Mohamed Bazoum.