Jeshi la Magereza lakemea kauli aliyoitoa Manara
Jeshi la Magereza Tanzania limesema limesikitishwa na kauli iliyotajwa kuwa isiyo ya kiungwana iliyotolewa na Haji Manara kwa jeshi hilo baada ya mechi ya Yanga SC dhidi ya Tanzania Prisons katika uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Magereza imesema Manara alikuwa akizungumza na waandishi wa habari huku akiwa ameegesha gari lake mbele ya gari ya Jeshi la Magereza na kwamba kwakuwa alikuwa amelizuia gari hilo, aliombwa kusogeza gari lake na kuruhusu gari hilo liweze kupita.
“ Hata hivyo, pamoja na kuombwa alikataa kwa dharau na kuanza kutoa maneno yasiyo ya kiungwana yenye viashiria vya kutweza utu na yenye mwelekeo wa kulifedhehesha Jeshi la Magereza,” imesema taarifa.
Aidha, Jeshi hilo limetoa onyo na kuwataka wananchi kuacha kutoa kauli zenye mwelekeo wa kubeza, na kudharau mamlaka yake au kulifedhehesha na kwamba halitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayehusika.