Kufuatia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kueleza kuwa hakuna uthibitisho unaoonesha kuwa viongozi wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) wanashikiliwa na polisi na kuamuru viongozi hao kutafutwa mahali walipo, Jeshi la Polisi limesema limepata taarifa za uhakika kuhusu viongozi wa chama hicho kupanga vitendo vya kiuhalifu vitakavyohatarisha amani.
Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, imesema viongozi wa CHADEMA wamefanya kikao kwa njia ya kielekroniki (zoom) na kukubaliana waanze kuhamasisha wafuasi wa chama hicho kufanya maandamano ya kuelekea maeneo mbalimbali zikiwemo ofisi mbalimbali.
Sambamba na hilo, taarifa hiyo imesema walipanga kuhamasisha na kuunda vikundi vya vijana wapatao 20 wavamie vituo vya polisi vilivyopo jijini Dar es Salaam kwa wakati mmoja.
“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa yeyote atakaye endelea kuratibu, kuhamasisha na kushiriki katika uhalifu huo wakupangwa ambao lengo lake ni kutaka kuvuruga amani ya nchi yetu baada ya kushindwa kwa mikakati yao, atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria za nchi,” imeeleza taarifa.
Aidha, taarifa hiyo imesisitiza kuwa “yeyote atakayefika kituo chochote cha Polisi kwa nia ovu, tumejiandaa na atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria. “