Jeshi la Polisi: Kauli ya RPC Theopista kuhusu binti aliyefanyiwa ukatili si msimamo wa Jeshi la Polisi

0
105

Jeshi la Polisi limesema kauli aliyoitoa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Theopista Mallya kuhusu binti aliyefanyiwa ukatili kuwa ‘alikuwa kama anajiuza’ si msimamo wa Jeshi la Polisi.

Kauli hiyo imefuatia baada ya RPC kuzungumza na chombo cha Habari hapa nchini kwa njia ya simu ambapo aliulizwa ikiwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na swali lingine aliloulizwa ni madai ya binti huyo kujiuza ambapo majibu ya kamanda huyo alisema hata kama ni hivyo hangestahili kutendewa hivyo.

“Jeshi la Polisi lingependa kuomba radhi kwa kila mmoja aliyeguswa na kuchukizwa na kauli hiyo inayosambaa kwenye vyombo vya Habari wakati ufuatiliaji ukifanyika kupata usahihi wake,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema wakati wa uchunguzi huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi amemhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Theopista Mallya Kwenda Makao Makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP George Katabazi.

Send this to a friend