Jeshi la Polisi lapiga marufuku kampuni za ulinzi kutumia Gobore

0
58

Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku kampuni binafsi za ulinzi kutumia silaha zilizotengenezwa kienyeji aina ya gobore kinyume na sheria.

Akitoa taarifa hiyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema katika siku za karibuni, Jeshi la Polisi limebaini kuwepo kwa baadhi ya kampuni binafsi za ulinzi kumiliki silaha aina ya Gobore bila kuwa na vibali kinyume na utaratibu wa sheria unaozitaka kampuni za ulinzi kumiliki shotgun kwa ajili ya shughuli za ulinzi.

“Jeshi la Polisi linatoa muda wa miezi miwili kuanzia tarehe 1/7/2024 hadi 31/8/2024 na baada ya kipindi hicho kutakuwa na msako mkali ambapo kampuni binafsi ya ulinzi itakayokutwa ikimiliki silaha hizo itachukuliwa hatua za kisheria,” ameeleza.

Aidha, amesema wananchi waliokuwa wakimiliki silaha hizo kwa kutumia leseni zilizotolewa na halmashauri za Miji na Manispaa, walielekezwa kuendelea kulipia silaha zao katika ofisi za Wakuu wa Polisi Wilaya (OCD) mpaka watakapoamua kutoendelea kumiliki au kutokana na sababu nyingine ikiwemo kifo, na kwamba silaha hizo hazitamilikishwa kwa watu wengine, bali jeshi litaziteketeza.

Send this to a friend