Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano na mikusanyiko ya aina yoyote yaliyopangwa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Mbeya kwa mwamvuli wa kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo imesema hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii wameonekana na kusikika baadhi ya viongozi wa CHADEMA wakihamasisha vijana kote nchini, viongozi wa kitaifa wa chama, kamati kuu ya CHADEMA na kualika baadhi ya watu kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kuadhimisha siku ya vijana mkoani Mbeya.
Polisi imesema pamoja na mwaliko huo, viongozi hao wa CHADEMA wameendelea kutoa kauli ambazo hazioneshi kuwa na lengo la kuadhimisha siku ya vijana duniani bali kwenda kuhamasisha kufanya vitendo vinavyolenga uvunjivu wa amani kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya.
Jeshi limeeleza kuwa miongoni mwa kauli hizo zinazoashiria kuvuruga amani ni za Katibu mwenezi BAVICHA Taifa, Twaha Mwaipaja ambayo amenukuliwa akisema kuwa “Kama kijana yeyote unaipenda nchi yako ya Tanzania, umeshalia miaka yako yote siku hii ya Agosti 12 tunakwenda kuweka hatma ya taifa letu la Tanzania mkoani Mbeya, kwa hiyo kijana yeyote uliyepo popote Tanzania njoo uwanja wa Ruanda Nzovwe Mbeya.”
Kauli nyingine ni “ Tupo serious sana na jambo hili kwahiyo vijana wote wa CHADEMA kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, siku ya Agosti 12 tunakwenda kuacha uteja kwa Serikali, na kuweka maazimio makubwa ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Kufuatia kauli hizo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kali na katazo kwa mtu au kikundi cha watu kinachojipanga kufanya maandamano na mikusanyiko kuacha mara moja, kwani Jeshi hilo liko imara na limejipanga vizuri kuzuia na kupambana na viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.