
Jeshi la Polisi nchini limesema hadi sasa hali ya kiusalama ni shwari na shughuli za kiuchumi na za kijamii zinaendelea vizuri katika mazingira ya amani.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelee kutii sheria sambamba na kushirikiana kulinda na kuimarisha amani kwakuwa kila mmoja anaihitaji katika maisha na katika shughuli za kila siku.
“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vinaendelea kuwaahidi tutaendelea kulinda usalama wa nchi yetu sote, maisha na mali za kila mmoja ndani ya Taifa letu la Tanzania,” imeeleza taarifa.
Imeongeza kuwa “Tuendelee kuelimishana na kuhimizana kuyakataa yale yote yanayo hamasishwa kwa njia mbalimbali na katika maneno ya kubadilisha mbinu kila mara ili kutaka kutuchonganisha na kutujengea chuki kati yetu lengo lao likiwa ni kutuingiza katika vurugu ambazo matokeo yake siyo mazuri kama tunavyo shuhudia katika maeneo mengine duniani.”







