Jeshi la Polisi latoa tahadhari kuelekea mchezo wa Simba na Yanga

0
24

Kuelekea katika mchezo wa Simba na Yanga Jumapili Aprili 16 mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam limetoa tahadhari na onyo kwa baadhi ya mashabiki wenye tabia za kufanya fujo ikiwemo kuwashambulia waamuzi wasaidizi wanaokuwa katika mechi hizo.

Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Jeshi la Polisi halitavumilia tabia iliyojengeka kwa baadhi ya mashabiki kurusha chupa za maji huku baadhi ya chupa hizo zikiwa na haja ndogo pamoja na uharibufu wa viti na mabomba ya maji.

Yakubu: Uwanja wa Benjamini Mkapa unatumika sana

Ameongeza kuwa tayari jeshi limekwishachukua tahadhari za kiusalama kabla na wakati wa mchezo huo, ikiwa ni pamoja na mifumo ya ufuatiliaji kwa mashabiki, na kusisitiza hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya vitendo vilivyo kinyume na taratibu.

“Ni marufuku kwa mtu yeyote kwenda na silaha ya aina yoyote kwenye uwanja ule isipokuwa vyombo vya dola ambavyo baadhi yao wataruhusiwa kwa ajili ya kazi za kiusalama,” amesema Muliro.

Aidha Jeshi la Polisi limewaondoa hofu wananchi kuwa ulinzi utaimarishwa ndani na nje ya uwanja, na kuwakumbusha mashabiki wote kuacha tabia ya kuhudhuria mechi wakiwa na matokeo mfukoni.