Jeshi la Polisi nchini limewaonya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaokusudia kukusanyika kinyume na sheria ili kumpokea kiongozi wa chama hicho anayerejea nchini Julai 27 mwaka huu.
Taarifa ya jeshi hilo imeeleza kuwa kukusanyika ni haki ya kila Mtanzania lakini hakuna haki isiyokuwa na wajibu na hivyo limewataka wananchi kutokiuka sheria kwani hakuna mamlaka iliyotoa kibali cha kuidhinisha tukio hilo.
Aidha, jeshi hilo limesema kuwa limeona kwenye mitandao ya kijamii wanaojiita viongozi wa wanafunzi wakihimiza wenzao kugoma na kutoingia madarasani kuanzia Julai 27 ili kushinikiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kurejea masharti ya mkopo kati ya taasisi hiyo na mnufaika wa fedha za kujikimu.
Polisi wamewataka wote wenye jambo lolote wafuate sheria, kanuni na taratibu kutafuta ufumbuzi na sio kuitisha migomo na maandamano.
“Ifahamike kuwa hivi sasa nchi yetu tunashughulika na jambo moja kubwa la kuomboleza kifo cha Rais wetu Benjamin Mkapa na hatutegemei wala Watanzania hawategemei kuona mtu yeyote anayekosa busara na kuanzisha mambo mengine yaliyo kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi,” imeeleza taarifa ya Polisi.