Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa saba kwa tuhuma za kupanga njama, kumtishia kwa silaha na kumteka mwanamke aliyefahamika kwa jina la Hani Nooh Hussein (29) mkazi wa Masaki, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi mkoani Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema tukio hilo limetokea Oktoba 16, 2023 saa nne asubuhi eneo la Msasani Village wakati mwanamke huyo akiwa anaendesha gari lake aina ya Toyota Rav4, na ndipo aliposimamishwa na sehemu ya kundi la watuhumiwa hao na kuingia ndani ya gari kisha kumtishia kwa silaha, kumteka na kuelekea maeneo ya Mbezi Beach.
Kamanda amesema walimshikilia kwa nguvu mwanamke huyo kwa siku nne huku wakidai pesa kwa vitisho kwa baba wa mhanga huyo kuwa asipotoa kiasi cha dola za kimarekani milioni 3.5 [TZS bilioni 8.7] mtoto wake atauawa.
“Jeshi la Polisi mara baada ya kupata taarifa ya tukio hilo lilifanya kazi ya ziada ya ufuatiliaji wa kisayansi na tarehe 19 Oktoba 2023. Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumwokoa mhanga na kuwakamata watekaji wote wakiwa na gari walilomteka nalo pia silaha iliyotumika Pistol Glock 19 yenye namba LZB 614 iliyotengenezwa Austria ikiwa na risasi 4,” amesema.
Utafiti: Dar yaongoza kwa wanawake kuharibikiwa mimba
Aidha, watuhumiwa waliokamatwa ni Hassan AbusherNur (39) Raia wa Canada mwenye asili ya Somalia, Nathan Lungumisa (27), Fredick Chahonza (49), Assad Abdurasur (43), Fahad Mussa (32), Ilfan Saleh (41), Nicolas Nilay (39) ambao wote wanatarajiwa leo kufikishwa katika mahakama ya Kisutu kwa hatua za kisheria.