Jeshi la Polisi Wilaya ya Tanga limezuia mkutano wa hadhara uliotarajiwa kufanyika Septemba 20, 2024 Tanga Mjini ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Tundu Lissu.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Polisi wilayani humo imesema zuio hilo ni kutokana na sababu za kiusalama, kwani mkutano huo unalenga kufanya maandalizi ya kufanya maandamano Septemba 23, 2024.
“Kwa mujibu wa mamlaka niliyonayo kutokana na K/F 44 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi sura ya 332, ninazuia uwepo wa mkutano kwani una dalili za kuleta uvunjifu wa amani ndani ya wilaya na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao,” ameeleza.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema kukiukwa kwa maelekezo hayo ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.