Jeshi la Polisi: Maandamano ya CHADEMA yasingekuwa ya amani kama walivyosema

0
69

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limewakamata watu 14 wakiwemo baadhi ya viongozi wa CHADEMA ambao ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.

Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema watu hao walikaidi agizo la Jeshi la Polisi la kutofanya maandamano ya kudai watu waliopotea na kuuawa yaliyopangwa kufanyika Septemba 23, ambapo amesema maandamano hayo yasingekuwa ya amani kama ambavyo walisema.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa ambao wamekaidi tamko la Jeshi la Polisi wakiwa wanaendelea kuyapanga lakini kutaka maandamano hayo ambayo tayari Jeshi la Polisi lilikwishapiga marufuku kwa sababu ambazo Jeshi ilizitoa,” ameeleza.

Aidha, amesema Watanzania wapuuze taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani kuwa watu hao wametekwa bali wamekamatwa na wanaendelea na mahojiano ili taratibu za kisheria ziendelee.

“Baada ya ufuatiliaji wa baadhi ya kauli zilizokuwa zikitolewa na viongozi wakuu wa chama hicho, tuliona vinaashiria kutokea kwa uvunjifu wa amani,” ameongeza.

Kamanda Muliro amesema kuhusu madai yanayotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika kuwa anasakwa na Jeshi la Polisi baada ya kushindwa kuripoti polisi kuhusu upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa kiongozi wa CHADEMA, Ally Kibao si za kweli na kwamba jeshi hilo litamkamata na kumhoji kwakuwa hana umuhimu wa kusakwa.

Send this to a friend