Jeshi la Polisi: Maandamano yaliyopangwa ni uhaini

0
56

Jeshi la Polisi limewaonya vikali watu wanaofanya vitendo vya uchochezi katika mitandao ya kijamii kwa kupanga maandamano ya kuiangusha Serikali ya Awamu ya Sita kuacha mara moja.

Akizungumza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillius Wambura amesema kuna taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazohusisha hoja za bandari ambapo kundi hilo linawashawishi wananchi kuunga mkono maandamano ya nchi nzima ili kuiangusha Serikali kabla ya mwaka 2025.

“Tuliamini hoja za bandari hujibiwa kwa hoja, na vile vile tukaamini kwa sababu baadhi ya watu walikwenda mahakamani, basi wangeheshimu maamuzi ya mahakama. Lakini badala yake wametoka na kuanza kutafuta ushawishi na kuwataka Watanzania waingie kwenye maandamano, mmoja amekwenda mbali zaidi na kusema watahakikisha wanaangusha Serikali ya Rais wa Awamu ya Sita kabla ya mwaka 2025, huu ni uhaini,” amesema.

Ameongeza kuwa, uchochezi unaofanyika ni kosa la jinai, hivyo Jeshi la Polisi halitawavumilia wote wanaoshiriki katika uchochezi huo, na kuwaomba wananchi wawapuuze watu hao kwani Tanzania ni nchi salama na yenye amani.

“Jeshi letu la Polisi ni jeshi imara sana, wasitikise kiberiti. Kama waliwahi kutikisa wakaguswa kule nyuma, wasiende hatua nyingine, huku wanakoshawishi kwenda ni sehemu mbaya sana. Ninawaonya wasijaribu tena kuendelea kufanya ushawishi na uchochezi huo,” amesema.

Ameongeza, “hatukubaliani na aina yoyote ya uhalifu wowote ule, tulitegemea kama kuna malengo ya kisiasa basi yaende kwenye hoja za kisiasa, yasitoke kule yakarudi kwenye matendo yoyote ambayo ni ya kihalifu.”

Send this to a friend