
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kukamata boti iliyokuwa ikisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini Kenya kupitia Bahari ya Hindi eneo la Mawe Mawili, Kijiji cha Kwale mpakani mwa Wilaya ya Mkinga na Jiji la Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi amesema boti hiyo ya rangi nyeupe aina ya fibre, ilinaswa na Kikosi cha Polisi Wanamaji kufuatia taarifa za kiintelijensia pamoja na ufuatiliaji wa kina kuhusu mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji haramu.
Ingawa watuhumiwa wawili waliokuwa kwenye boti walitoroka walipofika karibu na fukwe, boti hiyo pamoja na shehena ya mirungi vimekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.
Kamanda Mchunguzi amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalum katika maeneo ya baharini ambayo mara kwa mara hutumiwa kama njia ya kupitisha bidhaa haramu kutoka mataifa jirani.
Aidha, amewahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu hasa vinavyohusu biashara haramu ya dawa za kulevya ili kuilinda jamii na kuimarisha usalama wa taifa.







