Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema limeanza kufanya ufuatiliaji na uchunguzi wa taarifa ya kupotea kwa kijana Shadrack Chaula (24) mkazi wa Kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe mkoani Mbeya ambayo inasambaa katika mitandao ya kijamii.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema wamepokea taarifa ya kutoweka kwa kijana huyo Agosti 02, mwaka huu kutoka kwa baba mzazi wa kijana huyo aitwaye Yusuph Chaula (56), hivyo limeanza kufanya uchunguzi wake na kuwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki.
Aidha, limetoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo kijana huyo aziwasilishe kwa njia iliyo sahihi kwa viongozi wa Jeshi la Polisi ili kufanikisha kuwapata watu waliomchukua kijana huyo ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Shadrack ni kijana aliyeachiwa huru hivi karibuni baada ya kuchangiwa na wananchi faini ya TZS milioni 5 kufuatia hukumu yake ya miaka miwili au faini hiyo kwa kosa la kuchoma picha ya Rais na kusambaza taarifa za uongo mtandaoni.