Jeshi la Polisi: Tuna mamlaka ya kuzuia maandamano ikiwa yanahatarisha amani

0
47

Jeshi la Polisi limesema litaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mtu, au kikundi cha watu, kiongozi wa chama cha siasa au wafuasi wao wanaopanga, wanaohamasisha au wanaotenda vitendo vya kiuhalifu vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema imeona taarifa katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu na makundi mbalimbali akiwemo Wakili Boniphace Mwabukusi, Rais wa wa Chama cha Mawakili Tanganyika wakitoa maoni kuwa Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kuzuia maandamano ya vyama vya siasa isipokuwa wana wajibu wa kuyasimamia na kuyasindikiza kuhakikisha kuwa yanafanyika kikamilifu.

“Kutokana na hayo, Jeshi la Polisi linapenda kutoa ufafanuzi kwamba, Sheria ya Vyama vya Siasa sura 258 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019, kifungu cha 11 (7) (c) kinaeleza kuwa endapo mkutano au maandamano yanaonesha au yamedhamiriwa kusababisha uvunjifu wa amani au kuathiri usalama wa umma katika eneno hilo, Mkuu wa Polisi ambaye amepokea taarifa ya mkutano au maandamano hayo atatoa zuio la kufanyika kwa mkutano au maandamano hayo kwa mujibu wa kifungu cha 11 (6) cha sheria hiyo” imeeleza.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa “ Endapo chama cha siasa kitawasilisha taarifa ya kufanya mkutano au maandamano na Afisa wa Polisi wa eneo husika akawaandikia barua ya kuzuia mkutano au maandamano hayo, kwa mujibu wa Kifungu cha 43(6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi Wasaidizi, Sura ya 322 kama ilivyorejewa mwaka 2002, kinaelekeza kuwa chama husika kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.”

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa rai kwa wananchi kuwa ili kuweza kuelewa vema masuala ya kisheria ni vema kusoma sheria husika sambamba na sheria zinginezo.

Send this to a friend