
Televisheni ya taifa ya Sudan imeripoti kuwa Jeshi la Sudan liko karibu kuchukua udhibiti wa Ikulu ya Rais mjini Khartoum kutoka kwa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF.
Usiku wa Jumatano, mapigano makali yalizuka karibu na ikulu, huku mashuhuda wakiripoti milipuko na mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi katika maeneo ya katikati mwa Khartoum.
RSF iliteka Ikulu na sehemu kubwa ya mji mkuu wakati vita vilipoanza Aprili mwaka 2023, huku jeshi likipambana kuzuia kundi hilo kuchukua mji wa al-Fashir.
Kama jeshi litafanikiwa kuchukua mji mkuu, huenda likafanikiwa kudhibiti Sudan ya kati, jambo ambalo linaweza kugawanya nchi kati ya Mashariki na Magharibi.
Mgogoro huo ulianza baada ya wanajeshi wa pande zote mbili kufanya mapinduzi mwaka 2021, na baadaye vita vikazuka kufuatia mvutano juu ya mpango wa kurejesha utawala wa kiraia.