Jiko la mkaa laua mama na mwanae Njombe

0
66

Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Ashura Hatibu (20) na mtoto wake, Hamfrey Komba (3) wakazi wa Mtaa wa Buguruni mjini Njombe wamekutwa wamefariki kutokana na jiko la mkaa alilokuwa ameacha mama huyo wakati akipika njegere katika mgahawa alikokuwa akifanya kazi.

Akizungumza mama mzazi wa Ashura, Belutina Ndone amesema walifika katika mgahawa uliopo Mji Mwema alikokuwa akifanya kazi na kukuta mlango wa mgahawa umefungwa, hatua iliyowalazimu kubomoa mlango.

Ameeleza baada ya kubomoa mlango huo walimkukuta Ashura akiwa ameshafariki huku akiwa amekumbatiana na Mtoto wake.

“Tulipobomoa mlango na kuingia tulikuta pia alikuwa ametengeneza maandazi huku ikiwa imebandikwa mboga kwenye kigai, tulipoingia chumba alicholala kwa kuwa hakina mlango tukamkuta amelala na mwanae amemkumbatia na simu yake ikiwa pembeni na mkono mmoja alikuwa ameshika hela na mwingine amemkumbatia mtoto,” amesema mama wa marehemu.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Buguruni, Yolanda Ngulo ametoa wito kwa jamii kuwa makini na moto unaotokana na jiko la mkaa na kuomba wanaotumia majiko hayo hasa wakati huu wa baridi kuhakikisha wanazima jiko na kuweka nje ya nyumba inapobidi kabla ya kwenda kulala.

Send this to a friend