Jinsi mitandao ya kijamii inavyoweza kukusababishia upweke

0
6

Katika dunia ya leo yenye mitandao ya kijamii, simu janja, na teknolojia, inaonekana ni rahisi kuwa karibu na watu, lakini jambo la kushangaza watu wengi wanahisi upweke kuliko wakati mwingine wowote.

Upweke siyo tu kukosa watu karibu, bali ni hali ya ndani ya kutopata uhusiano wa kweli au kueleweka. Unaweza kuwa katikati ya umati wa watu lakini bado ukajihisi mpweke.

Mitandao ya kijamii inaweza pia kuchangia kwa kiasi kikubwa hali ya upweke. Hapa chini ni maelezo ya jinsi hali hii hutokea:

Kulinganisha Maisha na Wengine
Watu wengi huchapisha kwenye mitandao picha na habari za mafanikio, furaha, na maisha mazuri. Unapoangalia haya kila siku, unaweza kuhisi kuwa huwezi kufikia viwango hivyo, hata kama hali halisi si kama inavyoonekana mtandaoni.

Hali hii hupelekea mtu kujiona mdogo, aliyepitwa, au asiye na maana, na hivyo kusababisha upweke wa ndani.

Mahusiano Bandia
Marafiki mtandaoni ni wengi, lakini wengi wao hawana uhusiano wa karibu au wa kina. Matokeo yake, mtu huweza kuwa na mawasiliano mengi mtandaoni lakini asiwe na mtu hata mmoja wa kuzungumza naye kwa kina.

Hupunguza mikutano ya ana kwa ana
Maongezi ya kina hujenga mahusiano ya kihisia kitu ambacho jumbe za maandishi pekee haziwezi kutoa. Kukosa kuonana ana kwa ana kunaweza kuacha pengo kubwa la kihisia.

Kupoteza Muda mwingi Pekee Yako
Watu wengi hutumia muda mwingi wakiperuzi mitandaoni, muda ambao ungeweza kutumika kushiriki shughuli za kijamii au hata kujijali binafsi. Mwisho wa siku, mtu hukaa muda mrefu bila mwingiliano na wengine, na kuhisi upweke.

Kukosa Mwitikio wa Kihisia
Ukimwambia mtu “siko sawa” kwenye mitandao, unaweza kujibiwa tu na emoji au “pole”, si mazungumzo ya kina. Hii inaweza kufanya mtu ahisi kuwa haeleweki au hajaliwi, hivyo kuongeza hali ya kujitenga na jamii.