Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu amejitokeza hadharani katika kituo cha redio na kukanusha tuhuma zilizomuondoa madarakani kwa kudai kuwa tuhuma hizo hazina ukweli.
Raibu ambaye aliondolewa madarakani kwa tuhuma za kutumia vibaya nafasi yake, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuruhusu ujenzi holela na ukosefu wa adabu dhidi ya madiwani wenzake, amesema mtu yeyote mwenye ushahidi kwamba alikula rushwa apeleke taarifa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Dodoma: Wazazi watoa rushwa watoto waachishwe shule wakafanye kazi za ndani
“Nataka niwahakikishie sijawahi kula rushwa hata shilingi moja. Kama kuna mtu ana ushahidi huo sasa hivi aende, na kama hana nauli nitamsaidia,” amesema.
Kauli ya Raibu imekuja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa kueleza kuwa siku chache zijazo atatoa uamuzi wa rufaa uliokatwa na Meya huyo wa zamani.