JWTZ yatangaza nafasi za ajira kwa vijana

0
27

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kujiunga na Jeshi kwa vijana wa Kitanzania ambao wamemaliza mkataba wa mafunzo ya kujitolea JKT na kurudishwa majumbani, wenye elimu ya kuanzia kidato cha nne hadi shahada ya uzamili.

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema mwombaji anatakiwa awe Mtanzania wa kuzaliwa mwenye kitambulisho cha taifa, pia awe na umri wa miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha nne hadi kidato cha sita, na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.

Amebainisha kuwa mwombaji awe na afya nzuri na akili timamu mwenye tabia na nidhamu nzuri, awe hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai mahakamani na asiwe ameoa au kuolewa.

Upande wa vyeti, mwombaji anatakiwa kuwa na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya shule na vyeti vya taaluma, awe hajatumikia Jeshi la Polisi, magereza, chuo cha mafunzo au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, pia awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mkataba wa kujitolea miaka miwili na kutunukiwa cheti.

Aidha, Luteni ameelekeza maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi Dodoma kuanzia Machi 09 hadi Machi 20, 2023 yakiwa na viambatanisho ikiwemo nakala ya kitambulisho cha taifa au namba ya
NIDA, nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo, nakala ya cheti cha JKT pamoja na namba ya simu ya mkononi ya mwombaji.

Send this to a friend