
Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamtafuta mtuhumiwa wa mauaji ya Lillian Daniel (27), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Changalawe wilayani Kilosa.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema marehemu alikuwa na uhusiano na mtuhumiwa anayetafutwa, wakiishi pamoja kama mke na mume, lakini baadaye mwanamke huyo hakuonekana tangu Desemba 2025.
“Baada ya jitihada za kumtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio, ndugu walichukua uamuzi wa kukagua nyumba waliyokuwa wakiishi kwa lengo la kupata taarifa zozote zinazoweza kusaidia kumpata marehemu. Wakati wa ukaguzi huo ndipo ilipogundulika kuwepo kwa kaburi ndani ya nyumba hiyo,” imesema taarifa.
Imeongeza kuwa Machi 9, 2026 kaburi hilo lilifukuliwa na kukutwa mwili wa mwanamke anayedhaniwa kuwa ni Lilian. Hata hivyo Polisi wamesema uchunguzi wa kisayansi unaendelea ili kuthibitisha utambulisho wa mwili huo pamoja na kukamilisha hatua za kisheria.









