Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Ali Abeid Karume amewekwa chini ya uangalizi wa miezi mitatu na chama hicho kutokana na kauli zake alizozitoa za kukidhalilisha chama na viongozi wake.
Hatua hiyo inatokana na onyo alilopewa na kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Jimbo la Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja iliyokutana mwezi Juni 15, mwaka huu.
Karume aliitwa kuhojiwa na kamati ya maadili ya jimbo hilo kutokana na kauli zake alizozitoa kwenye mitandao ya kijamii, akikituhumu chama kuwa hakijawahi kushinda kihalali kisiwani humo na kumkosoa hadharani Rais Hussein Mwinyi kuhusu sera zake za kukodisha visiwa.
Pia alipinga utaratibu wa wananchi wa Kilimani kuondolewa kujenga ukumbi wa kimataifa na ujenzi wa uwanja wa Amani akidai vinakiuka utaratibu.
Waraka wa Jaji Stella Mugasha akipinga Rais kumuongezea muda Jaji Mkuu
“Pamoja na mambo mengine kikao kilipokea taarifa kutoka kamati ya maadili ya jimbo kuhusu mahojiano yaliyofanyika juu ya Ali Abeid Karume na kamati ya maadili ya jimbo, pamoja na makosa yake aliomba msamaha katika kikao hicho, kimeamua kukupa onyo kwa kukiuka maadili ya chama chetu,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Juni 11, katika moja ya mikutano yake, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi aliiagiza kamati ya maadili kuwashughulikia makada wanaokwenda kinyume na taratibu huku akihoji kwanini bado wako ndani ya chama.
“Wakati umefika kwa kamati ya maadili kufanya kazi yake, una sababu gani ya kubaki kwenye chama hiki, ikiwa hupendi chama ondoka! Nenda ukaseme hayo maneno ukiwa nje ya chama, unahoji hata ushindi wa CCM!” aliwaambia wafuasi bila kumtaja mtu.
Chanzo: Mwananchi