Kafulila afafanua sababu za kukatika kwa umeme licha ya Bwawa la JNHPP kuelekea ukingoni

0
4

Licha ya zaidi ya asilimia 90 ya ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere kukamilika, tatizo la kukatika kwa umeme bado linaendelea kutajwa, ambapo changamoto za miundombinu ya usafirishaji na usambazaji zimetajwa kuwa zinaweza kuchangia kukatika kwa umeme.

Akizungumza katika mahojiano na Wasafi FM, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila, amesema kuwa tatizo la umeme si suala la uzalishaji pekee, bali pia linahusisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji.

“Umeme ni vitu vitatu; kuna uzalishaji, usafirishaji na usambazaji. Kama kuna baadhi ya maeneo yenye miundombinu dhaifu ya usafirishaji au usambazaji, inaweza kusababisha tatizo la umeme katika hilo eneo, hata kama kuna ziada ya umeme,” amesema Kafulila.

Mbali na hilo, Kafulila ameeleza kuwa, pamoja na Tanzania kuwa na ziada ya umeme, ununuzi wa umeme kutoka nchi jirani unaweza kuwa wa manufaa kwa maeneo ya mipakani, pale ambapo gharama za kusafirisha umeme kutoka vyanzo vya ndani ni kubwa kuliko kununua kutoka nje ya nchi, akitolea mfano nchi zilizoendelea kama Marekani, Ujerumani na Norway ambazo licha ya kuwa na uzalishaji mkubwa wa umeme, bado hununua umeme kutoka nchi jirani.

Ameongeza kuwa kwa sasa, serikali inaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme ili kuhakikisha nishati hiyo inawafikia wananchi kwa uhakika.