Kamanda Muliro: Hakuna mtu aliyekamatwa, tuliwazuia kwa mahojiano

0
29

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Jeshi la Polisi halijawakamata waandamanaji waliojitokeza kushiriki maandamano leo jijini Dar es Salaam bali wamewazuia kwa muda kwa ajili ya mahojiano.

Akizungumza leo Juni 19, 2023, Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi limewazuia ili kufanya uchunguzi zaidi pamoja na kujua sababu za kutangaza maandamano hayo na kutoa mabango ambayo baadhi yalikuwa ya kejeli.

“Misingi yetu mikubwa ya kazi ya leo haikujikita katika ukamataji, tulijikita zaidi katika kuhakikisha kwamba utulivu unakuwa umeimarika. Kusema ukweli utulivu ulikuwa wa hali ya juu,” amesema Kamanda Muliro.

Kuhusu kushikiliwa kwa viongozi wa maandamano hayo amesema “Sisi tumefanya kazi ya uchunguzi, baadhi ya vijana waliotaka kujitokeza tumewazuia, tumewahoji na tumeongea nao vizuri, wametueleza vizuri, sasa hayo ni mambo ya kiuchunguzi.”

Aidha, Kamanda Muliro amesema hakuna nguvu yoyote iliyotumika wala hasara yoyote iliyotokea na kuongeza kuwa watu hawakujitokeza wengi kama walivyotarajia viongozi hao wa maandamano.

“Ujumbe wangu ni kuwashukuru sana wananchi, wananchi wengi wa Dar es Salaam wana uelewa mkubwa, wamepima mambo, wamefuatilia kwa ukaribu kwa hiyo ule uhamasishaji uliokuwa unafanyika ukiangalia na mrejesho wake unaweza kugundua kabisa watu wana uwezo mkubwa sana wa kufikiri,” ameongeza.

Send this to a friend