Kamanda: Mwalimu alimchoma kisu mwalimu mwenzake mbele ya wanafunzi darasani

0
60

Mwalimu wa Shule ya Msingi Igaka wilayani Geita, Emmanuel Chacha (35) amefariki dunia baada ya kuchomwa kisu na mwalimu mwenzake, Samwel Subi (35) akidai ni kikwazo cha maendeleo yake.

Akizungumza na Swahili Times Kamanda wa Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema tukio hilo limetokea Machi 15, 2023 saa 3 asubuhi ambapo walimu hao wawili walikuwa darasani wakiandaa mitihani ya darasa la pili, na ndipo mtuhumiwa alipochomoa kisu na kumchoma mwenzake kwenye chembe cha moyo mbele ya wanafunzi na baadhi ya watu waliokuwepo eneo hilo.

“Baada ya kufanya tukio hilo akajaribu kukimbia lakini baadaye tulifanikiwa kumkamata, na katika mahojiano alikiri kufanya tukio hilo, na kwanini alimuua mwenzake, akasema alimwona ni kikwazo cha maendeleo yake ya kazi,” ameeleza kamanda.

Mume ajinyonga ukweni baada ya mkewe kugoma kurudi nyumbani

Mtuhumiwa huyo ambaye inaelezwa kuwa hana muda mrefu tangu ahamie kwenye shule hiyo akitokea Shule ya Msingi Bukoli ambako pia alihamishwa kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri na walimu wenzake, amedai tangu ahamie shuleni hapo aliona kuwa marehemu ndiye kikwazo cha maendeleo yake kwani kulikuwa na nafasi ya uongozi ambayo alikuwa akiitamani.

Aidha, Kamanda Jongo amesema kwa upande wa wanafunzi ambao waliingiwa na taharuki kubwa baada ya kushuhudia tukio hilo wamedai waalimu hao walikuwa hawapatani, na muda mwingi walikuwa wakitupiana maneno.

Amesema Mwalimu Chacha alifariki wakati akipatiwa matibabu kwenye kituo cha afya cha Kasamwa, na kwamba hakuna mtu mwingine aliyedhurika kutokana na tukio hilo huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Send this to a friend