Kamati iliyoundwa kupitia tozo zilizopo kwenye mafuta
Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuchunguza upandaji wa bei za mafuta tayari imeshaanza kazi na imepewa siku 14 (hadi Septemba 16) kukamilisha kazi hiyo na kutoa majibu serikalini juu ya yale itayoyabaini.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuwa kamati hiyo itakaangalia maeneo matano ambayo ni mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja, mfumo wa ukokotoaji wa bei za mafuta na utaratibu wa serikali wa ununuzi wa mafuta kwa pamoja.
Maeneo mengine ambayo kamati hiyo inatarajiwa kutupia jicho lake ni kuangalia tozo mbalimbali zilizomo kwenye mafuta na utaratibu unaotumika kwenye bandari za Dar es Salaam na Mtwara ambako ndiko mafuta husushwa.
Msigwa ameeleza lengo la serikali ni kuangalia meneo ambayo yanaweza kushughulikiwa ili Watanzania wapate mafuta kwa bei nafuu, kwani kupanda bei ya mafuta kuna athari kwenye maisha ya watu na uchumi kwa ujumla.
Kamati hiyo imeundwa baada ya serikali kusitisha kutumika kwa bei mpya za mafuta kwa mwezi Septemba na kuagiza bei zilizotolewa mwezi Agosti kuendelea kutumika.