Kamati ya Bunge: Serikali idhibiti wavamizi wa mgodi wa Barrick Gold North Mara

0
54

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeagiza serikali kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti kundi la vijana wanaopanga mbinu ya kuvamia mgodi wa Barrick North Mara na kuchukuwa mawe yanayodhaniwa kuwa na madini ya dhahabu.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, David Mathayo wakati kamati hiyo ilipotembelea mgodi huo uliopo wilayani Tarime mkoani Mara ili kujionea shughuli zinazofanywa kwenye mgodi huo ambapo imeomba serikali ya mkoa huo kulinda uwekezaji huo ili kujenga nchi.

“Haiwezekani watu wamekuja hawana wasiwasi wamebeba mabegi na mapanga yao wanaingia wanafanya hivi na hivi halafu baadaye tunasema tumezidiwa. Serikali ipo ina vyombo vya aina mbalimbali, tunaomba hivyo vyombo hivyo vya aina mbalimbali viweze kubaini hivyo vitu kabla havijatokea, kwa sababu tunajirudisha nyuma wenyewe lakini tuharibu picha ya nchi,” amesema mwenyekiti.

Aidha, Kamati hiyo pia imeeleza kuridhishwa na jinsi Kampuni ya Barrick Gold inavyotekeleza Sheria ya ‘Local Content’ na hivyo kuwezesha Watanzania wengi wakiwemo wazawa wanaoishi jirani na migodi yake kunufaika na uwekezaji wake kupitia biashara na ajira.

Nao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wameipongeza Barrick kwa kuendelea kuleta mapinduzi kupitia uwekezaji mkubwa wa sekta ya madini nchini na kushauri mgodi huo uangalie uwezekano wa kuwasaidia wachimbaji wadogo ili wajikwamue kiuchumi kwa kuwapatia baadhi ya maeneo.

Kwa upande wake Meneja wa Barrick nchini, Melkiory Ngido amesema Barrick kupitia mpango wake ujulikanao kama The Barrick-Twiga Future Forward Education Programme, imetoa takribani TZS bilioni 70 kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya shule za sekondari ikiwemo mabweni pamoja na madawati katika maeneo mbalimbali nchini.

Send this to a friend