Kamati ya Ushauri Tanga yaidhinisha mapendekezo ya kugawa majimbo ya uchaguzi

0
6

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu, Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Tanga (RCC) imeidhinisha mapendekezo ya kugawa majimbo matatu ya uchaguzi: Kilindi, Handeni Vijijini, na Muheza, kila moja kuwa na majimbo mawili katika uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Jimbo la Kilindi litagawanywa na kuongeza Jimbo jipya la Songe. Handeni Vijijini litakuwa na majimbo mawili, Handeni na Kabuku, huku Muheza ikipendekezwa kuwa na majimbo mawili ya Muheza Mjini na Muheza Vijijini.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, ameeleza kuwa majimbo ya Kilindi na Handeni Vijijini yamekidhi vigezo vya ugawaji kutokana na idadi ya watu na mazingira yao, na kwa upande wa Muheza, idadi ya watu bado haijafikia vigezo vya Tume ya Uchaguzi vinavyohitaji jimbo kuwa na angalau wakazi 400,000 ambapo kwa sasa halmashauri hiyo ina wakazi 250,000.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando, amesisitiza kuwa ukubwa wa eneo la Jimbo la Handeni Vijijini, lenye kilomita za mraba 6,453, unasababisha changamoto katika upatikanaji wa huduma, hivyo kuligawa kutasaidia kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Idrisa Mgaza, ameeleza kuwa ongezeko la watu na uhamiaji kutoka Ngorongoro limeongeza mahitaji ya huduma, na tayari wilaya hiyo imepokea zaidi ya kaya 100 huku nyumba 1,000 zikiendelea kujengwa. Hivyo, kuongeza kata mpya ni hatua muhimu kwa utoaji wa huduma bora za kijamii.