Kamati yaundwa kuchunguza madaktari waliofeli mtihani

0
14

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameunda kamati huru ya uchunguzi ili kuchunguza malalamiko juu ya mitihani ya usajili iliyotolewa na wawakilishi wa madaktari waliohitimu mafunzo ya utarajali (interns) ili kutoa mapendekezo yatakayopelekea kutatuliwa kwa changamoto zitakazobainika.

Hatua hiyo ni baada ya wizara kupokea nakala ya barua ya wazi Julai 23, mwaka huu iliyoandikwa na wawakilishi hao ikielekezwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, huku ikiwa imeainisha hoja kadhaa zinazohusu malalamiko juu ya mitihani ya usajili kabla na baada ya utarajali inayotolewa na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT).

Kamati hiyo yenye wajumbe 13 ikiongozwa na Prof. Muhammad Bakari (Mganga Mkuu wa Serikali Mstaafu) itafanya kazi kwa kipindi cha mwezi mmoja, na katika kipindi hicho cha uchunguzi, taratibu nyingine za mafunzo ya watarajali zitakuwa zikiendelea kama ilivyoainishwa kwenye sheria.

Waziri Ummy ameongeza kuwa watarajali wenye changamoto tofauti na changamoto hiyo au inayoendana na hiyo wawasilishe changamoto hizo kwa Baraza la Madaktari ili kupata msaada zaidi.

Utafiti: Asilimia 63 ya Watanzania wanafurahia Serikali inavyosimamia uchumi

“Nihitimishe kwa kuwasihi madaktari tarajali wawe na subira katika kipindi hiki ambacho kamati itakuwa inafanya uchunguzi, na pale watakapohitajika kutoa maelezo mbele ya kamati watoe ushirikiano unaostahili. Aidha, niwahakikishie kuwa wizara itasimamia haki na ustawi wa taaluma ya madaktari nchini,” amesema.

Send this to a friend